Tuesday, May 13, 2014

NINI HATMA YA WASICHANA WALIO TEKWA NIGERIA

Marekani kutafuta mateka Nigeria

 
Marekani kusaidia kuwasaka wasichana waliotekwa na Boko Haram
Marekani imesema inapeleka vifaa vya uchunguzi nchini Nigeria kusaidia katika juhudi za kuwatafuta wasichana wanaozuiliwa na kundi la Boko Haram.
Wasichana hao walitekwa nyara kutoka shule moja Kusini mwa eneo la Borno mwezi mmoja uliopita.
Msemaji wa Rais Obama Jay Carney amesema kikosi cha maafisa 30 kiko nchini Nigeria tayari kushiriki juhudi hizo.

Mzazi Nigeria

"Ni heri watuonyeshe maiti za wasichana wetu badala ya kuwazuilia vichakani. Hili ni swala la hisia za ubinadam. Sisi hatuwezi kwenda kuwaokoa, wanajeshi hawawezi kwenda huko. Ni heri kutumia nguvu. Tukiona maiti zao mioyo yetu itakua huru"
Amesema msaada huo wa Marekani kutoka wizara za mambo ya nje na ulinzi na pia kutoka idara ya uchunguzi ya FBI.
Hatua hiyo imechukuliwa wakati baadhi ya Jamaa za wasichana waliotekwa nyara wakielezea majonzi baada ya kutazama kanda ya video iliyotolewa na kundi hilo.
Baadhi wameiambia BBC kuwa kanda hiyo imewapa matumaini lakini wameshangaa kuona wasichana hao ambao wengi ni Wakristu wamevalia mavazi ya Kiislam.
Akizungumza kwa uchungu nduguye mmoja wa wasicha waliotekwa ameiambia BBC ni heri kanda hiyo ingeonyesha maiti za wasichana hao kwa kuwa hiyo ingeondoa wasiwasi unaoendelea kukithiri na kuumiza mioyo ya wengi.
Kwenye kanda hiyo ya video kiongozi wa Boko Haram , Abubakar Shekau anasikika akiambia serikali ya Nigeria yuko tayari kubadilishana baadhi ya wasichana hao na wafuasi wake waliofungwa jela.
Hatahivyo wizara ya mambo ya ndani ya Nigeria imetupilia mbali pendekezo hilo.
Seneta Ali Ndume kutoka eneo ambapo wasichana hao walitekwa nyara anaisihi serikali kulegeza msimamo.