Kwa nini wahutu waliwaua watutsi?
Asilimia 85 ya wananchi wa Rwanda ni
wa kabila la Hutu, lakini jamii ya Tutsi imekuwa ikishikilia nyadhifa
kubwa tu za ngazi za juu kwa miaka mingi.
Mwaka 1959, wahutu walimuondoa mamlakani mfalme
wa Tutsi huku maelfu ya watu wa kabila hilo wakikimbilia nchi jirani
kama vile Uganda.
Kikundi cha watutsi waliokuwa ukimbizini
kikaunda vuguvugu waliloliita RPF ambalo lilivamia Rwanda mwaka 1990
huku vita vikiendelea hadi mwaka 1993 ambapo makubaliano ya amani
yalifikiwa.
Lakini usiku wa terehe 6 Aprili mwaka1994, ndege
iliyokuwa imewabeba hayati Rais Juvenal Habyarmana na mwenzake wa
Burundi Cyprien Ntaryamira ilidunguliwa.
Kila mtu aliyekuwa katika ndege hiyo alifariki.
RPF kilisema kuwa ndege hiyo iliangushwa na wahutu kama kisingizio cha
mauaji kufanyika.
Waume waliwaua wake zao kwa hofu ya wao kuuawa
Mauaji ya Kimbari yalifanyika vipi?
Kwa mpangilio wa hali ya juu. Orodha ya majina
ya waliokuwa wanapinga serikali ilitolewa kwa wapiganaji ili waweze
kuwaua pamoja na familia zao.
Majirani waliuana na hata waume wa kabila ta Hutu kuwaua wake zao wa Tutsi wakisema kuwa wangeuawa ikiwa wangetaa kufanya hivyo.
Wapiganaji walitumia vitambulisho vya watu
kuwaua kwani majina yao yalionyesha ikiwa walikuwa wahutu au watutsi.
Maelfu ya wanawake walifugwa kama watumwa wa ngono
Jumuiya ya kimataifa ililaumiwa pakubwa kwa kutizama tu mauaji yalipokuwa yanaendelea Rwanda
Nani alijaribu kusitisha vita?
Umoja wa Mataifa na Ubelgiji zilikuwa na
wanajeshi wao nchini Rwanda. Lakini umoja wa Mataifa haukuwa na idhini
ya kusitisha mauaji.
Mwaka mmoja baada ya wanajeshi wa Marekani
kuuawa Somalia, Marekani ilijitahidi kadri ya uwezo wake kujizuia
kuingia katika vita barani Afrika.
Wanajeshi wa Ubelgiji walilazimika kuondoka nchini humo baada ya kumi kati yao kuuawa.
Walituhumiwa kwa kutofanya juhudi za kumaliza
vita. Rais Paul Kagame ametuhumu Ufaransa kwa kuhusika na mauaji hao
ingawa Ufaransa imekanusha vikali madai hayo.
Vita vilimalizika vipi?
Chama cha RPF kikisaidiwa na Uganda , kilianza
kudhibiti sehemu kadhaa za nchi hiyo hadi Julai tarehe 4, wanajeshi wake
walipoingia mjini Kigali.
Wahutu milioni mbili wengi wakiwa raia walikimbilia nchi jirani ya DRC wakihofia kushambuliwa kama hatua ya kulipiza kisasi.
Watu milioni mbili wa kabila la Hutu walikimbilia nchi jirani kuepuka kisasi cha watutsi
Vipi hali ya Rwanda sasa?
Rais Paul Kagame na chama chake RPF amesifiwa kwa kurejesha utulivu nchini Rwanda na hata kukuza uchumi wa nchi hiyo ndogo.
Pia amejaribu kuifanya Rwanda kuwa nchi inayong'aa kiteknolojia.
Lakini wakosoaji wake wanasema kuwa hapendi kukosolewa huku vifo vya wapinzani wake vikileta shaka.
Takriban watu milioni mbili walihukumiwa katika
mahakama za jadi, viongozi wa mauaji wakihukumiwa katika mahakama maalum
kuhusu mauaji ya Rwanda mjini Arusha Tanzania.
Kwa sasa ni hatia kwa mtu yeyote kuzungumzia
ukabila nchini Rwanda, serikali inasema hii inasaidia kuzuia kutokea
tena kwa mauaji kama hayo, lakini wakosoaji wa serikali wanasema hiki ni
kiini macho tu kwani hisia zilizopo kuhusu ukabila huenda zikasababisha
hali nyingine mbaya baadaye ikiwa watu hawatapewa uhuru wa kuzungumza.