Monday, June 20, 2016

Simba wamshindwa Okwi

MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili wa klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amesema hawana mpango wa kumsajili kwa mara nyingine mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda Emmanuel Okwi, kwa sababu tayari kuna wachezaji wanafanya mazungumzo nao kutoka Ivory Coast na Zimbabwe.
Hans Poppe, alisema Okwi ni rafiki yao mkubwa na anakubali uwezo wake, lakini mazingira ya kumsajili kutoka kwenye klabu yake anayoichezea hivi sasa ya Sonderjyske ya Denmark ni magumu ndiyo maana wameona kuachana naye na kutafuta wachezaji wengine ambao wapo huru na wale wa bei nafuu.
“Okwi ni mchezaji mzuri lakini kwa bajeti yetu hatutaweza kumsajili kwa sababu pesa ambazo tungemsajili yeye kutoka Denmark tuna uwezo wa kupata wachezaji wazuri tena zaidi yake kutoka mataifa ya Ivory Coast, Zimbabwe na kwingineko Afrika,” alisema Hans Poppe.
Kiongozi huyo alisema pamoja na Mganda huyo, kuichezea kwa mafanikio timu yao na kuwa na mapenzi makubwa na Simba, lakini wameona ni vyema wakaliweka swala lake pembeni huku wakipambana kutafuta wachezaji wengine ambao itakuwa ni mara ya kwanza kucheza Ligi ya Tanzania na wanahitaji kupata mafanikio ili kujenga majina yao.
Alisema wao kama viongozi wamekubaliana wasisajili wachezaji kutoka mataifa ya Uganda na Kenya kutokana na usumbufu wanaoupata mara kwa mara na hiyo ni sababu nyingine inayowafanya kuliweka pembeni jina la Okwi kwa sababu msimu ujao wamepania kurudisha heshima yao na siyo malumbano na wachezaji.
“Msimu uliopita tulikuwa na wachezaji watatu kutoka Uganda, tuliona shida yake kitu ambacho naweza kusema kimechangia kututoa kwenye mbio za ubingwa, tumejifunza na tusingependa mambo kama hayo yakajitokeza tena kwenye timu yetu ndiyo maana tumeona safari hii tubadili twende mataifa mengine yaliyopiga hatua zaidi kisoka,” alisema.
Okwi anatajwa kutaka kurudi kwenye klabu ya Simba tena hata kwa mkopo baada ya kukosa furaha kwenye klabu hiyo ya Sonderjyske, ambako ameshindwa kuwika kama ilivyokuwa Simba ambapo aliweza kupataji jina kubwa na kujizolea umaarufu wa hali ya juu na kuwa kipenzi cha wana Msimbazi.

No comments:

Post a Comment