Monday, June 20, 2016

Nape aongoza mamia kufanya Yoga

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye jana aliongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam katika maadhimisho wa Siku ya Yoga Duniani kwa kushiriki kikamilifu kufanya mazoezi.
Nape aliwasili katika ufukwe wa Coco, ambapo maadhimisho hayo yalikuwa yakifanyika jana asubuhi na baada ya kuhutubia alitumia dakika kadhaa kufanya mazoezi hayo. Alikuwa na Balozi wa India nchini Sandeep Arya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambapo walipewa wasaa wao peke yao kwanza kufanya mazoezi hayo.
Baada ya hapo ilifika zamu ya watu wote waliokuwa viwanjani hapo kufanya mazoezi, ambapo pia Nape akiwa na Makonda, Balozi wa India hapa nchini pamoja na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Peter Kallaghe na wakazi wengine kuanza mazoezi hayo. Nape ambaye awali alisema kuwa alipokuwa akisoma nchini India alijifunza kwa ukaribu zaidi Yoga alionesha uwezo mkubwa wa kumudu mazoezi hayo.
Tukio hilo lililodumu kwa takribani dakika 35, ambapo waziri huyo pamoja na wenzake walifanya mazoezi hayo kwa umakini bila ya kupumzika. Walifanya mazoezi ya kunyonga miguu, kiuno, mgongo, mbavu, shingo pamoja na mazoezi mengine kama kuvuta pumzi kwa kutumia tundu moja la pua, mdomo na pamoja na mbinu nyingine za kuimarisha pumzi.
Kisha lilifuata zoezi la kunyanyua miguu juu, kufunga macho kisha kumalizia na kuomba. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa maadhimisho hayo, Nape alisema kuwa wizara yake itahakikisha kuwa inabainisha aina ya tamaduni zenye asili ya mazoezi ndani yake na kuziendeleza.
Alisema kuwa Yoga ilianza kama utamaduni wa India, ambapo kwa sasa umekuwa ni utamaduni mkubwa duniani na umekuwa ukiadhimishwa katika kila nchi zenye ubalozi wa India. Alisema kwa kuwa Yoga inalenga kuwaweka pamoja wananchi bila ya kujali tofauti zao za kidini, kabila, uraia hata jinsia, inaendana moja kwa moja na sera ya Tanzania.
“Yoga ni moja kati ya aina bora ya mazoezi ya kufanya ambapo inasaidia kuimarisha kila kona ya mwili, na mimi nimejifunza mengi kuhusiana na Yoga wakati nikiwa India ninasoma na leo nimejikumbushia mengi sana,” alisema Nape.
Kwa upande wake Balozi wa India hapa nchini, Sandeep Arya alionesha kufurahishwa na idadi ya wananchi waliojitokeza katika ufukwe huo na kuwataka kuendelea kujitokeza kwa wingi zaidi katika kituo cha Utamaduni cha India hapa nchini kinachotoa mafunzo hayo.
Alisema kuwa Yoga ni zaidi ya mazoezi kwa kuwa yanasaidia pia kuondoa msongo wa mawazo, kukuza namna ya kufikiria mambo na pia ni njia mojawapo ya tiba kwa baadhi ya magonjwa.
“Sisi India Yoga ni utamaduni na tena ni njia mojawapo ya kujiimarisha zaidi katika maisha ya kila siku kwa kuwa kwanza ni nidhamu na pia ni mfumo wa maisha ya kila siku tunayoishi kuanzia kula na mengineyo,” alisema balozi huyo.
Aliongeza: “Kwa hapa nchini kupitia kituo cha utamaduni kilichopo chini ya Ubalozi wa India, tunatoa mafunzo kwa kila atakaye kujifunza Yoga na watu wafike kufundishwa zaidi”.
Kwa upande wake, Makonda alitoa wito wa matumizi ya lugha ya Kiswahili pia katika utoaji wa mafunzo hayo ili kila mtu aweze kuelewa kirahisi zaidi mazoezi hayo kitu ambacho kilifanyika hapo Coco ambapo mbunifu wa mavazi nchini Ally Remtulah alikuwa akitafsiri maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na wataalamu wa Yoga kwa lugha ya Kiingereza na kuzungumza Kiswahili.
Mchezo huo umeonekana kupendwa na wengi na hata wale ambao bado hawajajiunga wameonesha nia ya kutaka kujiunga na huenda wengi wakajitokeza katika kituo hicho cha India kwa ajili ya kujifunza zaidi mchezo huo. Pia mchezo huo unaweza kumsaidia mtu kujiamini mbele ya maadui pale anaposhambuliwa na majambazi, waporaji au vibaka.

No comments:

Post a Comment